Fahamu kuhusu ukuaji wa mtoto kiakili

Mtoto huzaliwa na ubongo unaochemka vizuri ili kumwezesha kuyaelewa mazingira yake na hivyo kujenga kumbukumbu ya mambo anayokutana nayo bila kutegemea mafundisho/maelekezo yoyote.  Kwa kutumia taarifa zinazotoka kwenye viungo vya mwili wake na milango ya fahamu, mtoto anaweza kurekodi yanayoendelea kwenye mazingira yake ili kumsaidia kujifunza.

Kwa ujumla, katika miezi sita ya mwanzo, mtoto huwa na shughuli kubwa ya kujenga uzoefu unaofanana na vipande vya filamu kadri anavyoingiliana na wanaomzunguka kwenye mazingira yake. Ongezeko la vipande hivi vya filamu katika ufahamu wake ndivyo vinavyomsaidia kujenga uhusiano baina ya matukio na kadri unavyoongezeka, humsaidia kufikiri kwa ufasaha.

Hii ina maana kwamba anachofikiri mtoto huanzia kwenye kile kinachofanyika kwenye mazingira yake ikiwa ni pamoja na mwili wake mwenyewe. Hana uwezo wa kufikiri kisichoonekana kwa macho.

Kadhalika, milango yake ya fahamu inayoendelea kupevuka hutenda kazi sawa sawa kumsaidia mtoto kujenga tajiriba ya ufahamu pamoja na kwamba uwezo huo unaongezeka hatua kwa hatua. Kwa mfano, ndani ya miezi sita mtoto huwa na uwezo wa kurudia matendo ya mwili wake yanayoleta matokeo yenye kumvutia.

Kurudia kinachovutia ni hatua ya kwanza katika hujenga uwezo wa kumbukumbu na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika mazingira yake. Hiyo ndiyo kusema, wajibu wa mzazi ni kumwekea mazingira sisimushi yanayomfanya ajenge uwezo wa kutatua vikwazo katika mazingira yake kwa wepesi na uhuru.

Ndani ya mwaka mmoja mtoto huweza kukumbuka uwepo wa vitu asivyoviona kwa macho kuthibitisha kwamba kumbukumbu yake inaimarika. Katika kipindi hiki, hujenga uwezo wa kutafuta vilivyofichwa pamoja na kutambua sauti za watu anaowafahamu wanaomzunguka. Hii ni hatua kubwa sana ya kiakili inayoweza kuimarishwa kwa kumwekea mazingira sisimushi. 

Tukio jingine muhimu la ukuaji wa kiakili ni matumizi ya lugha katika kuwasiliana na wanaomzunguka kati ya miezi 12 na 18.  Mtoto huanza kutumia maneno katika kuwasiliana na wengine. Ingawa ni kweli kwamba idadi ya maneno yanayotamkwa huzidi ufahamu alionao mtoto, ongezeko la msamiati ni dalili ya kukua kwa uelewa wa mtoto. Mpaka anafikisha miezi 24, mtoto huwa na msamiati wa maneno zaidi ya 200 yanayowakilisha dhana, vitu, watu na hali kadha wa kadha katika ufahamu wake. Maana yake ni kwamba sasa mtoto huweza kufikiri kwa kutumia lugha bila kuhitaji kukiona kitu kwa macho.

Ongezeko la uwezo wa kujenga picha ya kinachozungumzwa bila msaada wa kuwepo kwa kitu halisi humsaidia kusikiliza hadithi fupi fupi na kuzielewa. Hiki ndicho kipindi ambacho mzazi anaweza kumsomea hadithi fupi kumfundisha dhana mbalimbali katika maisha kama kuelewa hisia za wengine, matokeo ya tabia zisizokubalika, nidhamu, mambo ya kiroho na kadhalika.

Kwa sababu ya kuimarika kwa uwezo wa kufikiri na kuhoji, mpaka anapofikisha miaka mitatu, mtoto huwa na uwezo wa kuuliza maswali mengi yanayolenga kumsaidia kuelewa mambo yanayomtatiza katika mazingira yake. Pamoja na kumwongezea msamiati wake na uelewa, maswali mengi ni mbinu ya kukuza mahusiano na wanaomzunguka. Ndio kusema, mzazi ana wajibu wa kuyajibu maswali ya mtoto kwa usahihi kulingana na umri wa mtoto.

    

Comments